DUNIA MAPITO

Kuna familia ya mjomba wangu imeishia pabaya sana. Najitahidi kuamini vinginevyo lakini akili yangu inaniambia ni laana.

Mjomba wangu alikuwa ni msomi wa Ph.D na alikuwa na pesa kama uchafu. Majumba, magari na miradi mingine kibao. Alikuwa na mke na watoto watano wa kike wawili na wa kiume watatu.
 
Watoto wote walikuwa wamesoma shule za maana, namaanisha za maana sio za umma ila shule za maana za kimataifa ambazo hata watoto wa mabwenyenye wangesoma bila shida. Vyuo baadhi yao wamesoma nchi za ng'ambo.

Mjomba alikuwa ni mtu mwenye upendo na alisaidia sana ndugu zake. Kiukweli alikuwa ni mtu ambaye ametoboa sana kimaisha ukilinganisha na ndugu zake wengine wa ukoo mzima.
 
Baadaye aliugua afya yake ikazorota sana na akili zikawa kama zimeruka kidogo (sio sana). Mkewe na watoto wake hawakumjali. Kila alilowaambia hawakumsikiliza akawa hana thamani tena. Huwezi amini mfanyakazi wa kiume wa nyumbani alimtunza na kumjali kuliko mkewe na kizazi chake. 

Kuna siku watoto wake waliuza mashine fulani kwa mhindi ambayo aliipenda sana. Siku mhindi amekuja kuinunua alikuwa juu ghorofani nyumbani kwake akiangalia, aliwakataza wasiiuze mpaka machozi yakamtoka, lakini hakuna hata aliyehangaika kujishughulisha kumsikiliza, huku mkewe akiwa ndio mhamasishaji mkuu.

Baada ya miaka kama mitatu alifariki dunia, inasemekana alifariki na kinyongo sana. Lakini kabla ya kifo aliacha wosia akazikwe kijijini kwao, lakini familia yake haikutekeleza hilo takwa lake.

Kipindi cha msiba ulitokea mgogoro mkubwa kati ya familia yake na ndugu washamba wa kijijini. Ndugu walitaka akazikwe kijijini na walikuwa tayari kuchangia gharama, lakini familia iligoma katakata.

Wakatokea wanasheria marafiki wa enzi za uhai wake huko jijini Nairobi wakatetea wakisema kisheria mke ana haki ya kuamua wapi mmewe akazikwe. Ndugu ikabidi wawe wapole na walivyo waporipori kusikia mambo ya sheria wakanywea.

Lakini walikuwa na kinyongo sana, maana walikusanyika kwa ajili ya kuzika na mwili haukuletwa. Hivyo wakaamua kwenda kutembelea sehemu ambayo kama angeletwa kijijini basi marehemu angezikwa. Sehemu hiyo kulikuwa na makaburi ya ukoo, unaambiwa wanandugu wakasafisha makaburi na kuomba dua ya kuwaombea laana wale watoto na familia ile.

Hivi majuzi  mtoto wa huyo mjomba aliyekuwa amebakia naye pia alipiga dunia teke. Mjomba alifariki 2010 yaani ndani ya miaka takribani kumi tu familia nzima imepukutika, amebaki mama naye afya yake inasikitisha.

Kinachosikitisha watoto watatu walibahatika kufunga ndoa, lakini wote hawakuwahi kupata watoto hata wa kusingiziwa. Familia yote wameingia kaburini bila watoto, mama yao kabaki peke yake bila hata mjukuu.

Mimi si Mungu ila naomba Mungu anisamehe kama nitatumia lugha isiyo na hekima wala nidhamu. Ila ukweli huyu mama ni wa leo wa kesho. Inasikitisha sana laana zipo jamani. NB familia bado haijafirisika, pesa bado ipo kama yote, ila waliopaswa kuifaidi wametangulia wote wakiwa bado vijana wadogo.

Hitimisho, tujitahidi kuishi vyema maisha yetu hapa duniani, maana tunaweza kukutana na kifo siku yoyote na siku hiyo inaweza kuwa leo.

Comments

Popular posts from this blog

KINDERGARTEN CLASS

DESIDERATA 💯